MITAA YA KATI (Bila Sanaa Ningekuwa Mkabaji MitaaYa Kati)-Imam Abbas ft Juma Nature
SAUTI YA KITAMBO KUTOKA MTAA
Hivyo ndivyo mashairi ya msanii mkongwe wa swahili Hip Hop, Imam Abbas
yanavyoanza kwenye nyimbo yake ya ‘Bila Sanaa’ mwaka 1999. Nadhani lile swali la
nini nafasi ya swahili Hip Hop katika jamii yetu litaanza kupata maana
kupitia nyimbo hii. Pamoja na bado wapo wajinga wachache katika vyombo
vya habari, wanaoita swahili Hip Hop, muziki wa kufokafoka, bila kujua hii
ni aina ya fasihi simulizi. Taswira ya fasihi katika nyimbo hii ni ya
kipekee, ambayo inaibua maswali muhimu na kuonesha mustakabali wa vijana
wa leo.
‘Bila sanaa’ inakupa mtazamo wa vijana walio wengi katika Tanzania ya leo, kwani maisha yao ni kama kuwa na “
panga shingoni”.
Panga hilo, laweza kuwa la kibaka akimwibia raia, au panga hilo laweza
kuwa mafisadi wanaodhoofisha maendeleo; hivyo rushwa zao na ubinafsi wao
ukizidi kuacha taifa lenye vijana wengi matatani.
Ugumu
wa maisha, hasa kwa vijana unatokana na sababu mbalimbali. Wale walio
bahatika, wakasoma na wenye vipaji, wanahemea kupitia elimu yao au sanaa
yao, kama hii ya Hip Hop. Lakini wengi wa vijana wapo kwenye fungu la
wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatari. Hao sasa, ndio wale ambao
kila siku wanatamani wangebaki “
utotoni”, kwani “
Bongo motoni;”
kwani wakiwa wezi kweli watachomwa moto.
Lakini kwanini tuishi kama tupo motoni? Mtu unabaki ukijiuliza, hivi
ukimya wetu vijana ndio unatufanya tuonekane mafala, au tumekubali
yaishe kuwa sisi ni watu dhaifu. Labda moja kati ya sababu kubwa
zinazotufanya
tusiamke, ni hofu kuwa, kelele zetu “
zitapotea kama moshi wa udi,” bila kusikiwa na hata kuleta mabadiliko yo yote.
Vijana waliosoma ni wachache, ajira zenyewe ni chache, na kwa wale ambao “
maisha piga mashuti,” wanajikuta wanashindana na
Wachina kwenye umachinga. Msanii II Proud enzi hizo aliuliza “
ni wapi tunakwenda, tu.. tunakwenda” kipindi hicho ambapo tabia ya kuzamia meli kwa vijana ndiyo ilikuwa imeshamiri. Leo hii uzamiaji meli sio
ishu tena, kwani tumekubali kubaki nyumbani na kuwa watumwa.
Sasa je, utumwa huu utakuja kufika kikomo? Hawa viongozi je, viongozi
wanaodharau vijana, wanaodharau mchango wa swahili Hip Hop kwa vijana na
jamii kwa ujumla, hivi hawajui hatari ya dharau zao? Leo hii, tunaweza
kuulizana maswali tu, ya “
tafakari je, ningevunja mlango wako, juu yake kibano, kisha vitu msanyo,”
kupitia nyimbo hii. Lakini, kesho ufisadi ukazidi, maisha ya vijana
yakazidi kuwa matatani, unadhani vijana tutabaki tu kuwa kwenye “
kona ya mtaa,” huku
“
moshi wa msuba unapaa, umeishia ukizubaa,”
au hata wao mafisadi watajikuta wakiwa wamewekewa mapanga shingoni.
Labda hilo ndilo tunalohitaji lifanyike, badala ya kugeuziana visu sisi
wenyewe kwa wenyewe.
Bila ubishi, sisi vijana na hao mafisadi tuishukuru sanaa, kwani
‘Bila Sanaa’, Imam Abbas anajadili maisha yangekuwa vipi; labda angekuwa
mkabaji, mteja, mwizi, muuaji, lakini pia Lupe Fiasco msanii wa Marekani ameweza kuandika baada ya miaka kumi,
Hip Hop Saved His Life.basi upeo wa imam utukuzwe
.
Mwisho, Imam Abbas anaonya kuwa, “
taifa la leo, majambazi wa kesho,”
kama viongozi hawatachukulia kilio cha vijana kwa umakini. Kwani siku
moja itatutabidi tujenge ukuta, wakati nyimbo kama ‘Bila Sanaa’,
zinatuwekea wazi nyufa ambazo zinatakiwa kuzibwa. Mwisho wa siku, ukweli
ni huu, matatizo ya vijana hayatatuliwa yote leo, kwani hata
Roma haikujengwa kwa siku moja. Lakini sasa, juhudi lazima zianze leo, kwani kama nchi hii
itateketea, basi sote tutateketea nayo, na tusisahau wala kudharau uwezekano huo.
Sikiliza nyimbo nyingine za Imam Abbas
Horses na
Sunshine. Pia unaweza kusikiliza wimbo wa Lupe Fiasco ‘
Hip Hop Saved My Life…’